Jumatano, 25 Mei 2016

Mwanza Kupokea Tani 500 Za Sukari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella, amesema mkoa wa Mwanza unategemea kupokea Tani 500 za Sukari zitakazo ingia katika mkoa huu zikitokea kiwanda cha sukari cha Kagera Sugar tarehe 24, Mei, 2016, ambazo zinaingizwa mkoani hapo na muagizaji na Msambazaji P.H  Shah.

Hata hivyo mkuu wa mkoa ameonya watu watakao uza sukari hiyo kinyume na bei elekezi kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja nakufikishwa katika vyombo vya dola.

Mongella amesema pia kwamba, kupitia kamati yakushughulikia sukari, tayari wametoa maelekezo kwa Wakuu wa wilaya jinsi yakushughulikia suala la sukari na kwamba wasambazaji wote katika Wilaya lazima wazingatie maelekezo bila kuvunja utaratibu utakao wekwa.

Mahitaji ya sukari katika mkoa wa Mwanza ni Tani 1,500 kwa wiki kwa matumizi ya kawaida kwa wananchi wake, hivyo kuwasili kwa tani 500 itasaidia kupunguza uhaba wa sukari  unao ukabili  mkoa huu kwa sasa..

Hata hivyo mkuu wa mkoa amewatoa wanachi hofu juu ya sukari kwakusema, tayari viwanda vya hapa nchini vimekwisha anza uzalishaji wa sukari na kwamba muda si mrefu tatizo la sukari litapungua kama sio kuisha kabisa.

Imetolewa na Atley J. Kuni
Afisa habari na Mahusiano, Ofisi ya mkuu wa Mkoa
MWANZA -24, Mei 2016

Viongozi Wa Africa Wataka Mahusiano Yaboreshwe Kwa Maendeleo Ya Bara

WAKUU wa nchi za Afrika wametaka kuwepo na juhudi za pamoja katika kukabiliana na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabiachi yanayolikumba bara hilo.

Kauli hiyo ilitolewa jana mchana (Jumanne, Mei 24, 2016) wakati wa majadiliano baina ya viongozi kutoka Zambia, Chad, Nigeria, Msumbiji na Tanzania mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa 51 wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano cha kimataifa wa Mulungushi, jijini Lusaka, Zambia.

Wakishiriki kwenye mjadala wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliohusu Nishati na Mabadiliko ya Tabianchi, viongozi hao walisema bara la Afrika linahitaji kupata maendeleo zaidi licha ya tatizo la nishati linalolikumba bara hilo hivi sasa.

Akichangia mjadala huo, Rais wa Zambia, Bw. Edgar Lungu alisema nchi yake imepania kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme vijijini lakini imekuwa ikikabiliwa na tatizo la uhaba wa mvua kwa zaidi ya miaka miwili hali ambayo alisema imechangia kukosekana kwa umeme katika maeneo mengi nchini humo.

“Uhaba wa mvua umepunguza kiwango cha maji katika bwawa la Kariba ambalo hutumika kuzalisha umeme nchini mwetu. Na hapa kwetu, karibu asilimia 80 ya umeme wetu, unategemea uzalishaji wa umeme kutokana na vyanzo vya maji,”  alisema.

Rais wa Chad, Bw. Idriss Deby Itno aliitaka benki ya AfDB ichukue nafasi ya mdau mkuu kwenye uwekezaji wa sekta ya nishati na kuzisadia nchi za bara hili kupata mitaji ya uwekezaji na ushauri wa kitaalamu.

“Tunahitaji kutumia fursa ambazo benki yetu inazo katika kukabilianana changamato za ukosefu wa nishati. Tukiweza kutekeleza jambo hilo, tutafanikiwa kuwa na miradi ambayo ni makini na kwa maana hiyo tutaweza kuliangaza bara letu la Afrika kwa kupata mwanga wa uhakika,” alisema.

Kwa upande wake, Makamiu wa Rais wa Nigeria, Prof, Yemi Osinbajo alisema bara la Afrika halina budi budi kuweka kipaumbele kwenye masuala ya maendeleo yake wakati likitafuta suluhisho la kukabiliana na athari za mazingira.

“Tunapaswa kutafuta njia za kubalance mahitaji makubwa ya umeme ambayo bara letu linakabiliwa nayo dhidi ya athari za kimazingira ambazo zinapigiwa kelele na mataifa makuna na zinahatarisha kutunyima fursa ya kuendelea haraka kama ilivyokuwa kwao,” alisema na kuongeza:

“Kama nchi zilizoendelea zinataka sana kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, zinatakiwa zitupatie fedha, teknolojia na wataalamu ambao watasaidia kuendesha mitambo ili tupate nishati safi kutokana na mafuta ya petroli na dizeli sababu ni rasilmali ambazo tunazo.”

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema ili kuondokana na tatizo la nishati, kuna haja ya kuwa na viongozi wenye utashi wa kisiasa ambao watakuwa tayari kuruhusu uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya nishati na kuongeza kuwa Tanzania inapitia upya sheria zake ili kuruhusu miradi mikubwa ya uwekezaji kwenye sekta hiyo.

Aliwaambia washiriki wa mkutano huo kwamba milango ya uwekezaji Tanzania iko wazi kwa ajili ya wawekezaji walio tayari kuwekeza kwenye sekta hiyo na kutaja fursa ambazo Tanzania inazo kwenye sekta ya nishati ikiwemo gesi asilia, makaa ya mawe, madini ya urani, maji, upepo na nishati ya joto kutoka ardhini (geothermal energy).

Naye Waziri Mkuu wa Msumbiji, Bw. Carlos Agostinho do Rosário alisema kuna haja ya kuwa na taasisi ya uzalishaji na ugawaji umeme ya pamoja (electricity pool) ambayo itaruhusu wazalishaji wa umeme wawauzie wanunuzi wakubwa.

Waziri Mkuu ambaye yuko Lusaka kuhudhuria mkutano huo wa ADB kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli, amerejea nchini leo (Jumatano, Mei 25, 2016).

Dk Shein Amuwakilisha JPM Comoro

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein anaondoka leo jioni kwenda Muungano wa Visiwa vya Comoro kwa ziara ya siku mbili.

Akiwa nchini humo Dk Shein atamuwakilisha Rais Dk John Magufuli katika sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa nchi hiyo, Azali Assoumani Boinakher.

Kuapishwa kwa Boinakher kunafuatia ushindi wake alioupata katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika tarehe 10 Aprili 2016 na ule wa marudio katika kisiwa cha Anjouan uliofanyika tarehe 11 Mei, 2016.

Sherehe hizo za kuapishwa Rais huyo mteule zitafanyika kesho katika kiwanja cha Mpira cha mjini Moroni na zinatarajiwa kuhudhuriwa  na viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi hiyo.

Katika ziara hiyo Dk Shein amefuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Bora , Issa Haji Ussi Gavu na Mshauri wa Rais Uhusiano wa Kimataifa, Uchumi na Uwekezaji Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.

Makampuni 52 Yajitokeza Kuwekeza Sekta Ya Umeme Bongo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi sasa Serikali imekwishapokea maombi 52 kutoka makampuni mbalimbali ambayo yanataka kuwekeza kwenye sekta ya umeme nchini Tanzania.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Mei 24, 2016) wakati akizungumza na Watanzania waishio Zambia katika mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini Lusaka, Zambia.

“Haya maombi yamekwishapokelewa na wenye makampuni wamekwishahojiwa kuangalia uwezo walionao katika suala zima la uwekezaji wanaotaka kuufanya, na tukiwapata wenye uwezo na wenye nia ya dhati watapatiwa miradi ya kuiendesha,” alisema.

Aliwataka Watanzania hao waishio Zambia watumie fursa ya uwepo wao huko kutafuta marafiki ambao wanaweza kuja kuwekeza kwenye miradi mbalimbali nchini kwani Serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu wakati wananchi wanahitaji kupatiwa huduma muhimu.

“Serikali peke yake haiwezi kufanya kazi ya uwekezaji kwa hiyo tunahitaji kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo na ndiyo maana kule kwenye mkutano nimewaeleza washiriki kwamba milango ya uwekezaji Tanzania iko wazi."

Alisema kupatikana kwa umeme wa uhakika kutawezesha wananchi wengi zaidi kujiingiza katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuinua uchumi wa nchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Alisema malengo ya Serikali ya awamu ya tano ni kuona kuwa nchi inakuwa na mitambo mingi ya kuzalisha umeme na umeme wote unaozalishwa na mitambo hiyo inaunganishwa na gridi ya Taifa ili kuondokana na tatizo la mgao wa umeme nchini.

Alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya nishati vikiwemo gesi asilia, makaa ya mawe, madini ya urani, maji, upepo, nishati ya joto kutoka ardhini (geothermal energy) na nishati inayotokana na vinyesi vya mifugo (biomass) ambayo alisema vinatumika kwa watu wachache (siyo kitaifa).

Alisema kupatikana kwa gesi asilia nchini kumeleta neema ambapo mabomba ya gesi yamekwishajengwa kutoka Mtwara hadi Kinyerezi na kutoka Kilwa-Songosongo hadi Dar es Salaam. 

“Sasa hivi kuna utafiti unaendelea juu ya uwezekano wa kusambaza gesi ya kupikia majumbani. Tumeanza pale Mikocheni (DSM) na sasa hivi wanafanya utafiti mwingine kule Mtwara ili wananchi waweze kutumia gesi hii kupikia badala ya mkaa,” alisema.

Akielezea kuhusu uwekezaji kwenye makaa ya mawe, Waziri Mkuu alisema Serikali imelenga kutumia makaa ya mawe ili kuendeshea mitambo ya kwenye viwanda vikubwa badala ya kutumia umeme au mafuta ya dizeli kama inavyofanyika sasa.

 “Baadhi ya wenye viwanda wanabadilisha mifumo ya kuendeshea mashine zao ili iweze kuendana na teknolojia ya makaa ya mawe pindi tu uchimbaji ukishika kasi,” alisema.

Akifafanua kuhusu juhudi za Serikali katika kusambaza nishati ya umeme, Waziri Mkuu alisema tangu kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), vijiji zaidi ya 3,000 katika ya vijiji 12,000 vilivyopo nchini vimefikiwa na nishati ya umeme.

“Tulianza na REA awamu ya kwanza, awamu ya pili na sasa tunaenda awamu ya tatu. Hata mkipiga simu kwa ndugu zenu vijijini, mtakuta katika kila kata kuna vijiji kati ya vinne hadi vitano ambavyo vimefikiwa na nishati ya umeme kupitia mradi wa REA,” alisema.

Waziri Mkuu amerejea nchini leo (Jumatano, Mei 25, 2016).

Jumapili, 22 Mei 2016

Tuhuma za Ubadhirifu wa Sh bilioni 1.4 za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana Zatua TAKUKURU


TUHUMA za ubadhirifu wa Sh bilioni 1.4 za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana, zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma, zimefikishwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga, alisema Takukuru inakamilisha uchunguzi wa kina ili wahusika waliofanya ubadhirifu huo wachukuliwe hatua za kisheria. 

Alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Alisema upo ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi uliofanywa na wahusika waliopewa dhamana ya kusimamia matumizi yake. 

Ngaga alisema, ofisi yake baada ya kuunda tume ndogo na kubaini hilo, uchunguzi wa awali unaonesha Sh milioni 513 zimefanyiwa ubadhirifu .

Alisema, aliona ni vyema achukue hatua ya kukabidhi tuhuma hizo kwa Takukuru wafanye uchunguzi wa kina kutambua ni nani aliyehusika na ubadhirifu huo.

 Alisema, taarifa na majina ya wahusika waliofanya hivyo itatolewa baadaye Takukuru ikikamilisha kazi yake.

“Takukuru inaendelea na uchunguzi, ikikamilisha taarifa itatolewa. Katika maelezo yangu ya awali kwenye Baraza la Madiwani lililokaa juzi sikuhukumu mtu wala kusema amehusika, hivyo tusubiri tutajulishwa,” alisema.

Aliongeza kuwa, uchunguzi huo utakapokamilika, taarifa husika zitapelekwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la Ulinzi na Usalama mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu awasilishe kwa Waziri mwenye dhamana.

Awali, tuhuma za ubadhirifu huo, zilitolewa na Mkuu wa Wilaya kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa wilaya hiyo, Mei 11, mwaka huu.

Familia Yasema Kifo cha Wilson Kabwe Hakikutokana na Mshtuko wa Kufukuzwa Kazi na Rais Magufuli


Familia ya Wilson Kabwe, aliyekuwa mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, imesema ndugu yao alishawatoa wasiwasi kuhusu tuhuma zilizosababisha kusimamishwa kazi na Rais John Magufuli na kwamba alitamani uchunguzi ufanyike haraka ili ukweli ujulikane. 

Kabwe aliyefariki dunia Mei 20 kwa ugonjwa wa saratani ya tezi dume jijini Dar es Salaam, alisimamishwa kazi na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa daraja la Mwalimu Nyerere lililopo Kigamboni Aprili 19. 

Miongoni mwa makosa yaliyosababisha kusimamishwa kwake ni madai ya kusaini mkataba kwa kutumia sheria ndogo ya mwaka 2004 kutoza magari yanayotoka kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo (UBT) Sh4000 na mwingine wa Sh8,000 chini ya sheria ndogo mwaka 2009. 

Kulikuwa pia na madai ya kukithiri kwa rushwa katika kituo hicho hasa katika kutoa magari na ukodishwaji wa vyumba vya kupangisha, kinyume na utaratibu na kuongeza muda wa mzabuni aliyeingia mkataba na jiji wa maegesho ya magari. 

Akizungumza jana nyumbani kwao, Masaki jijini Dar es Salaam, mtoto wa marehemu, Joseph Kabwe alisema kifo cha baba yao hakikutokana na mshtuko wa kusimamishwa kazi, bali alianza kuugua muda mrefu na alishawaambia kuwa hana wasiwasi na tuhuma hizo, bali anataka uchunguzi ufanyike haraka. 

“Alikuwa na saratani ya tezi dume na alikuwa akitumia dawa za chemotherapy ambazo ni kali sana na zilisababisha kuathirika kwa ini. Hata siku baba anatumbuliwa pale darajani alisema hana wasiwasi kwa sababu kila kitu kiko sawa sawa,” alisema Joseph. 

“Baba alitutaka tusiwe na wasiwasi, tena mwenyewe alikuwa akisisitiza kuwa anatamani matokeo ya uchunguzi yatoke mapema ili ukweli ujulikane,” alisema. 

Jana msibani kulikuwa na viongozi tofauti wa ngazi ya mkoa waliofika kutoa pole. Kaimu mkurugenzi wa jiji aliyekuwapo msibani hapo, Sarah Yohana alisema Halmashauri ya Jiji inashiriki msiba huo kwa kuwa Kabwe alikuwa mtumishi wao. 

“Yule alikuwa mtumishi wa halmahsauri na ana haki zake kama mtumishi mwingine yoyote. Tutatoa jeneza, gari la kusafirishia maiti, chakula na rambirambi,” alisema Sarah. 

Sarah alisema alikabidhiwa ofisi na Kabwe tangu Novemba mwaka jana baada ya kwenda kutibiwa nchini India. Kuhusu taratibu za utumishi, alisema licha ya Rais kumsimamisha kazi, hawakuwahi kuona barua yoyote iliyoletwa inayohusu kusimamishwa kwake. 

“Inawezekana alipewa kwa njia nyingine, lakini sisi hatukuona barua ya kusimamishwa. Yule ni ‘presidential appointee’ (mteule wa Rais), yeye ndiye mwenye mamlaka na watu wake wa kufanya uchunguzi. Sisi hatujui, inawezekana wanafanya uchunguzi wao huko wenyewe,” alisema Sarah. 

Jana Msemaji wa familia hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Eliab Mkenga Kabwe alisema hawana ugomvi wowote na Serikali huku akimkana mtu aliyejitambulisha kuwa msemaji wa familia hiyo, Dk. Zawadi Machuve aliyetoa maelezo kwa waandishi wa habari juzi kuwa hawataki viongozi wa Serikali wakanyage msibani. 

Aliongeza kuwa familia hiyo inatambua na kuthamini mchango wa Serikali katika kugharamia matibabu na huduma zote za mazishi. 

Alisema Makonda aliyetoa tuhuma za Kabwe kabla ya Rais Magufuli kutangaza kumsimamisha kazi, anatarajiwa kufika msibani hapo muda wowote. 

“Mkuu wa Mkoa, Makonda bado hajafika hapa, lakini anaweza kufika wakati wowote. Unajua yeye ndiye mwenye mkoa wake kwa hiyo atafika tu wakati wowote,” alisema.

Mbali na viongozi wa jiji waliokuwapo kwenye msiba huo, viongozi wa mikoa mingine akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo na mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga walikuwapo msibani hapo. 

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, ambaye alikuwapo eneo hilo, ameshauri msiba huo uhamishiwe katika ukumbi wa Karimjee ikiwa ni kumpa heshima Kabwe aliyekuwa kiongozi wa jiji, lakini hakuna dalili za kufanya hivyo.

CCM: Hatutamuadhibu Kitwanga Mara Mbili


CCM imesema kitendo cha Rais John Magufuli kumvua uwaziri Charles Kitwanga kutokana na kuingia bungeni akiwa amelewa, kimedhihirisha kuwa bado kuna baadhi ya watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma, lakini hakitachukua hatua kwa kuwa ameshaadhibiwa.

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka jana  alisema kitendo cha Kitwanga kuingia bungeni akiwa amelewa kimewapa fundisho na sasa wanajua kuwa kuna baadhi ya watumishi waliopewa dhamana na chama hicho, lakini wanakiuka miiko ya maadili ya utumishi wa umma, jambo ambalo ni kinyume na taratibu zao.

Sendeka alisema licha ya kwamba Rais Magufuli amechukua hatua juu ya hilo na kutoa adhabu, CCM itaendelea kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya wanasiasa waliopewa dhamana na chama hicho.

“Hatutasita kuchukua hatua endapo tutabaini kuna kada anayekiuka maadili ya viongozi wa umma,” alisema Sendeka.

Alisema CCM inampongeza Rais Magufuli kwa uamuzi aliochukua dhidi ya Kitwanga kwa kuwa hatua hiyo imedhihirisha kauli aliyowahi kusema kwamba hataangalia mtu usoni wala kujali kabila au dini, ikiwa mtu huyo atakiuka miiko ya uongozi.

Kuhusu CCM kumuadhibu Kitwanga, Sendeka alisema adhabu aliyopewa na Rais inatosha. “Hukumu haitolewi mara mbili,” alisema Sendeka.

Kitwanga ambaye anatajwa kwenye sakata la utekelezaji mbovu wa mkataba wa kufunga vifaa vya kuchukua alama za vidole baina ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises, alivuliwa ukuu wa wizara hiyo nyeti baada ya kutinga ndani ya ukumbi wa Bunge Ijumaa asubuhi na kujibu maswali akiwa amelewa.

Hadi jana jioni, Rais Magufuli alikuwa bado hajajaza nafasi hiyo nyeti huku wananchi wakibashiri jina la mrithi wa Kitwanga kwa kuangalia jinsi marais waliopita walivyokuwa wakijaza nafasi kama wa kumpandisha naibu waziri wa wizara hiyo au nyingine, kumteua mtu anayemfahamu, kubadilisha mawaziri na kumrejesha aliyewahi kuwa waziri ama kuteua kutoka kwenye kanda anayotoka aliyetimuliwa.

Mara nyingi katika uteuzi wa mawaziri, viongozi wakuu wa nchi wamekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya manaibu kuwa mawaziri, kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua au kuteua waziri kutoka katika mkoa ambao anatokea waziri aliyeondolewa.

Mara zote saba ambazo Rais mstaafu Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri alifuata utaratibu huo.

Alipomuondoa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye ni mbunge kutoka mkoa Kagera alimteua mbunge mwingine kutoka mkoa huo, Charles Mwijage kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.Kwa sasa Mwijage ni Waziri wa Viwanda na Biashara. 

Utaratibu huo unaweza kunufaisha wabunge sita wa majimbo yaliyopo mkoa wa Mwanza ambao ni Chalres Tizeba (Buchosa), Mansoor Hirani (Kwimba), Kiswaga Boniventura (Magu), Stanslaus Mabula (Nyamagana), William Ngeleja (Sengerema) na Richard Ndassa (Sumve).

Mbali na Kitwanga ambaye aliteuliwa kuwa waziri kutoka mkoa huo, Rais pia alimteua mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Iwapo Rais atatumia utaratibu wa kupandisha naibu waziri kuwa waziri, neema huenda ikamuangukia mbunge wa Kikwajuni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandishi Hamad Masauni au naibu mawaziri kutoka wizara nyingine. Katiba pia inampa Rais fursa ya kuteua wabunge 10 na tayari ameshatumia nafasi sita.